Friday, November 15, 2013
Friday, October 18, 2013
UPINZANI ‘WAWASHA MOTO’ ZANZIBAR,WATAKA CHIKAWE AJIUZULU
Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za uongo kwamba Zanzibar ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis Bakari wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliovishirikishwa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
Aboubakari alisema kwamba Zanzibar ilipokea taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu vifungu vinne vya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar itoe maoni na mapendekezo yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema vifungu vya mabadiliko ghafla viliongezwa kutoka vinne hadi 12 bila ya Zanzibar kupewa nafasi ya kujadili vifungu vinane ambavyo vina umuhimu mkubwa katika kupata katiba bora.
“Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai,” alisema Aboubakari.
Alisema kabla ya kufanyika Waziri akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, William Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka wajadili vifungu hivyo kwa siku moja jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
“Baada ya kuanza kupiga kelele, wenzetu walikuja Zanzibar wakitaka tujadili mabadiliko ya mswada,nikawaambia siwezi kujadili masilahi ya nchi kijuujuu, huko ni kuiuza nchi, siko tayari kufanya hilo,” alisema.
Aboubakari alisema marekebisho yaliyofanyika katika muswada huo na kutoa nafasi kujadili na kupitisha mabadiliko ya Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni sawa na wazimu.
Alisema mabadiliko yoyote ya Katiba yanapaswa kutumia theluthi mbili toka pande mbili za Muungano, utaratibu ambao ndiyo umekuwa ukitumika na nchi mbalimbali zenye mfumo kama wa Tanzania. Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kujibu tuhuma hizo alisema Aboubakari ameudanganya umma mchana kweupe kwa vile yeye na Waziri Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu ya muswada na si kujadili na kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe alisema kwamba walipokabidhi muswada pia walimtaarifu siku ya kuwasilishwa muswada huo katika kikao cha Bunge na kuwataka kutoa maoni na mapendekezo kwa wakati mwafaka kabla ya kujadiliwa na kamati ya Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema kwamba nyongeza ya marekebisho ya vifungu vinane yalitokana na mapendekezo ya wabunge katika kamati na michango ya wabunge ndani ya Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa kisheria.
“Baada ya kamati ya Bunge kukaa, Mbunge Halima Mdee wa Chadema ndiye aliyependekeza kutumika kwa utaratibu wa wingi wa kura katika kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba kama hatua ya theluthi mbili itashindwa kufikia mwafaka,” alisema Chikawe.
Pia alisema mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Jaku yeye alitetea kwa nguvu ya hoja kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize kazi yake baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Rais na kwamba haikuwa ni uamuzi na matakwa ya Serikali kama inavyodaiwa na vyama vya upinzani kuhusu nyongeza hiyo.
“Nyongeza ya vifungu ilitokana na wabunge katika kamati na ndani ya Bunge lenyewe, Serikali haiwezi kupuuzia ushauri wa wawakilishi wa wananchi na wabunge ambao wanaisimamia Serikali,” alisema Waziri Chikawe.
Aidha, Aboubakari alimshutumu Naibu Spika wa Bunge,Job Ndugai kwa kulidanganya Bunge kwa kitendo chake cha kutoa barua ikithibitishaZanzibar imeshiriki wakati kuna vifungu vya ziada vimefanyiwa marekebisho bila ya kupata baraka ya Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo amevunja na kukiuka kanuni za Bunge na wabunge wana haki ya kumshtaki kwa kutumia kanuni zao kwa kupotosha Bunge na umma.
Hata hivyo, taarifa hizo za Aboubakari kutokana na maelezo aliyotoa awali Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwenye mkutano wa hadhara, alisema Zanzibar ilishirikishwa katika kuvifanyia vifungu sita na SMZ ilitoa mapendekezo katika vifungu vitatu na baadae vikaongezwa vinane kinyemela bila ya Zanzibar kushirikishwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kwa muda mrefu viongozi wa Zanzibar walikuwa wakijitolea kupigania mabadiliko ya taifa lao na kukutwa na vizingiti ikiwemo kuwekwa vizuizini na kupewa hongo ya madaraka.
Mbatia alisema miongoni mwa viongozi waliojitoa muhanga kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano ni pamoja na Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi ambaye aliondolewa kibabe madarakani chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimtaka Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwa madai kuwa hawana nia njema wakikusudia kuharibu nia njema ya Rais ya kupata Katiba mpya.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema Katiba iliyopo sasa nchini haifai kwa kuwa imejaa upungufu unaokwenda kinyume na misingi ya haki za raia.
Chanzo:Mwananchi
Read More
Labels:
LOCAL NEWS
WARIOBA: SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA INA UPUNGUFU
Wakati wananchi wa kada mbalimbali wakishinikiza Rais Jakaya Kikwete kutokusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013, kwa maelezo kuwa una kasoro, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye amesema sheria ina upungufu.
Warioba alisema jana kwamba ni jambo la kushangaza sheria hiyo kueleza kuwa tume hiyo itavunjwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wakati huohuo ikieleza kuwa itahusika tena kusimamia utoaji wa elimu ya kura ya maoni.
Kauli hiyo ya Warioba imekuja wakati vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF, vikifanya mikutano nchi nzima kuwashawishi wananchi kupinga kile wanachokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya.
Sheria hiyo ambayo Warioba amesema ina upungufu, muswada wa marekebisho yake ulijadiliwa na kupitishwa wa wabunge Septemba 6, mwaka huu katika Mkutano wa 12 wa Bunge Mjini Dodoma, ikiwa ni baada ya kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu na hivi sasa Rais Kikwete anasubiriwa kuusaini ili iwe sheria kamili. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema: “Mwisho wa kazi ya tume ni baada ya kukabidhi rasimu, hilo ni tatizo. Maana tume itakuwa imeshavunjwa, sasa itafanyaje kazi ya kutoa elimu kwenye kura ya maoni?”
Jaji Warioba pamoja na kukiri upungufu huo, alisema kurekebisha au kutokurekebisha kasoro hizo si jukumu la tume hiyo.
“Tunawaomba watafakari, waone jinsi gani tume ambayo imekwishavunjwa itakuja kutoa elimu wakati wa kura ya maoni, sheria ina ‘contradiction’ (ina mkanganyiko),” alisema.
Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM baada ya wale wa upinzani kutoka nje baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kuamuriwa na Naibu Spika, Job Ndugai kutoka nje kutokana na kukaidi kwake amri ya kukaa chini alipokuwa akitaka kutoa hoja kabla ya mjadala wake kuanza.
Muswada huo unapingwa kwa kuwa Rais amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe 166, ambao si wabunge wala wawakilishi na Zanzibar kutokushirikishwa kikamilifu kwenye maandalizi ya muswada huo.
Hata hivyo, Warioba alisema pamoja na kasoro hizo Tume hiyo inafanya kazi yake kwa kufuata sheria hiyo huku akisisitiza, “Wanaotunga sheria ni wengine siyo sisi, tulipoteuliwa tulikuta sheria na kuanza kazi kwa kuifuata. Imefanyiwa marekebisho sisi tunafuata.”
Alisema waliofanya mabadiliko ya sheria hiyo wana haki ya kufanya hivyo na kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba haiwezi kuzuia kutokufanyika kwa mabadiliko hayo, kwani yapo baadhi yanaihusu.
Alisema baada ya kuipata sheria hiyo: “Tulijiuliza maswali kwa sababu miswada huwa inapelekwa bungeni na Serikali ikiwemo ya Katiba. Anayeipeleka kama ni waziri ndiye anayetoa ufafanuzi pale inapohitajika.”
Alisema kulingana na sheria, tume yake ndiyo inayotakiwa kutoa ufafanuzi katika Bunge la Katiba, kama ambavyo Waziri hutoa maelezo anapowasilisha muswada bungeni.
“Tulipouliza tulielezwa kwamba sisi ambao tumepewa jukumu la kupata maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ndiyo tutaitwa pale tu patakapohitajika ufafanuzi wa jambo fulani,” alisema.
Alisema kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba itafanyika na kukamilika katika muda uliopangwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Tulianza kazi Mei mwaka jana na tunatakiwa kumaliza Novemba mwaka huu, sheria inaruhusu kuongeza miezi miwili kama tutakuwa hatujakamilisha kazi. Katiba Mpya inatakiwa iwe imekamilika Aprili 26, 2014,” alisema.
Chanzo:Mwananchi
Read More
Labels:
KATIBA,
LOCAL NEWS
MUSWADA BINAFSI KUFUTA SHERIA YA MAGAZETI YA 1976
Na Zitto Kabwe
Napenda kuujulisha umma kwamba leo Ijumaa tarehe 4 Oktoba, 2013 nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi Bungeni kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Changamoto iliyopo ni Sheria mbadala ya vyombo vya habari baada ya Sheria ya sasa kufutwa. Hata hivyo wadau wa habari kama Baraza la Habari Tanzania wameshafanyia kazi suala hili kwa muda mrefu sana na wana mawazo kuhusu sheria mbadala. Nimejulishwa kuwa muswada wa sheria mpya ya habari tayari upo. Kwa hiyo katika mchakato wa kujadili muswada binafsi wa kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 mabadiliko yanaweza kufanywa ili kutunga sheria mpya. Hatua ya kwanza ni kuifuta sheria hii kandamizi ambayo kiukweli tumechukua muda mrefu sana na baada ya madhara makubwa kufikia hatua ya muswada wa kuifuta.
Nimeamua kutumia njia za kawaida za kuwasilisha muswada na kuepuka njia ya dharura ili kujenga mazingira ya wadau wa habari kushiriki vya kutosha katika mabadiliko yanayotakiwa. Njia ya dharura ni ya haraka lakini huziba fursa za kupata maoni ya wadau ambao kimsingi ndio wenye sheria yenyewe haswa. Hivyo nimepeleka muswada leo ili uchapwe kwenye gazeti la Serikali (GN) kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kisha usomwe kwa mara ya kwanza, uende kwa wadau kwa mjadala na marekebisho na kisha kusomwa kwa mara ya pili na kupitishwa na Bunge.
Ikumbukwe kuwa juhudi za kufuta sheria hii ni juhudi za wadau wa tasnia ya habari na ni juhudi walizofanya kwa muda mrefu sana. Mimi kama Mbunge ninawasilisha tu kwa sababu taratibu zetu za kuandika sheria zinataka ama Serikali, Kamati ya Bunge au Mbunge kuwasilisha muswada. Kwa muda mrefu tumewaangusha wana habari kwa kutosukuma vya kutosha mabadiliko waliyokuwa wanayapigania. Hata hivyo, kuna msemo wa kihindi ‘asubuhi huanza pale unapoamka’. Sasa tuchukue hatua za kufuta sheria hii kandamizi.
Zitto Kabwe,Mb
Kigoma Kaskazini
LINK: http://www.scribd.com/doc/173328345/Repealing-the-Newspapers-Act-1976
Read More
Labels:
SHERIA
DED Kiteto kuburutwa mahakamani
Na Mohamed Shaabani Manyara
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashari ya Wilaya ya Kiteto Bi. Janne Mutagurwa anakusudiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhalilisha Diwani wa kata ya Sunya Mussa Briton kuwa amekula fedha za ujenzi wa Sekondari Tsh laki sita na nusu.
Akizungumza hayo Diwani huyo baada ya kumalizika siku saba alizotoa kwenye kikao cha baraza la madiwani kumtaka mkurugenzi huyo kuthibitisha madai hayo alisema, kwa kuwa mkurugenzi ameshindwa kuthibitisha madai hayo yeye atamfikisha mahakamani
Alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuchafuliwa kisiasa kwa kutumiwa watendaji na nyaraka za Serikali kuwa amehujuma mradi wa ujenzi wa sekondari ya Sunya iliyopo wilayani hapo na kuongeza kuwa hakuhusika kufuja fedha hizo
“Kazi ya diwani ni kuhamasisha maendeleo ya kata yake ili yaweze kusonga mbele, mimi sio mhasibu wa kamati ya mradi wowote ndani ya kijiji au kata sasa inakuwaje nituhumiwe kuhujumu mradi tena kwa kuandikwa kwenye makabrasha ya vikao vya Halmashauri”?
“Kamati ya fedha na mipango imepitisha na kubariki kuletwa taarifa hii kwenye kikao cha madiwani, naamini walioyaleta hapa wana uhakika ya walichokiandika na kwa bahati nzuri taarifa hii ni ya mkaguzi wa ndani wa Halmashauri aliyotumwa na mkurugenzi ningependa sheria ifuate mkondo wake”Alisema Bw. Briton
Hata hivyo Diwani Braitoni aliliambia gaeti hili kuwa tayari amekwisha kuwasiliana na wakili wake ambaye kwa sasa wamepanga kuandika barua maalumu (notes) ya siku ishirini na moja kwa mkurugenzi ya kuonyesha nia hiyo ya kumshitaki kwa kushindwa kutimiza matakwa ya diwani huyo kusafishwa ndani ya kata yake
Aidha hoja hiyo ilivuta hisia kwa wawakilishi hao wa wananchi kwa kumtaka diwani huyo awe na subira na kuacha uamuzi wake huo wakisema kuwa uchunguzi wa kina ufanyike zaidi kubaini ukweli ya suala hilo ambalo lina taswira ya kuchafuliwa kisiasa
Akizungumza hayo Diwani Kone Lembile wa kata ya Kijungu alisema hakuna haja ya Diwani huyo kuhamaki kwani kama jambo hilo sio kweli haliwezi kuleta madhara kwake, lakini kama atakuwa amehusika hapo ndipo shida inaweza kutokea
Akiendelea na hoja hiyo huku akikatishwa na diwani huyo Lembile alisema, wananchi kwa nafasi zao nao hupima kinachozungumzwa na kumtaka diwani huyo kupuuza kauli hiyo ambayo inaonekana kuwa huenda kweli imemchafua kiasiasa
Hata hivyo hoja hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa Halmashaur i ya wilaya Mainge Lemalali kwa kumwomba Diwani huyo kuacha uamuzi huo akisema kuwa atahakikisha jengo hilo linakamilishwa na kuachana na mvutano huo wa kisiasa
“Mhe. Briton tukiachana na suala la umri nakusihi achana na uamuzi wako huo, kwani haya yataweza kuchelewesha maendeleo ya wananchi wakati tunaweza kukaa chini sisi na kutafuta ufumbuzi, ili mwisho wa siku tuone maendeleo ya wananchi yanasonga mbele”alisema Lemalali
Kauli hiyo ilizidi kuchochea hasira kwa diwani huyo na kutoa uamuzi wa mwisho kuwa mkurugenzi huyo apite katika vitongoji na vijiji katika kata yake hiyo ya Sunya kuelezea kuwa diwani huyo hakufuja fedha jambo ambalo mkurugenzi huyo hakulifanya
Hata hivyo gazeti hili lililazimika kuongea na mkurugenzi kuhusiana na tuhuma hizo na kusema kuwa ameshangazwa na uamuzi wa Diwani huyo wa kutaka kumfikisha mahakamani na kuongeza kuwa akiwa kama katibu wa madiwani hao atahakikisha kuwa wanayamaliza
Kuhusu kupita kwenye kata yake kutangaza kuwa diwani huyo hakuhusika na ufisadi mkurugenzi huyo alisema kuwa ni mapema na wala jambo hilo sio kubwa kama linavyo tafsiriwa na baadhi ya watu hasa wakidhani kuwa suala la kumfikisha mkurugenzi mahakamani ni rahisi
Read More
Labels:
LOCAL NEWS,
MAHAKAMA
Subscribe to:
Posts (Atom)