Na Mohamed Shaabani Manyara
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashari ya Wilaya ya Kiteto Bi. Janne Mutagurwa anakusudiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhalilisha Diwani wa kata ya Sunya Mussa Briton kuwa amekula fedha za ujenzi wa Sekondari Tsh laki sita na nusu.
Akizungumza hayo Diwani huyo baada ya kumalizika siku saba alizotoa kwenye kikao cha baraza la madiwani kumtaka mkurugenzi huyo kuthibitisha madai hayo alisema, kwa kuwa mkurugenzi ameshindwa kuthibitisha madai hayo yeye atamfikisha mahakamani
Alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuchafuliwa kisiasa kwa kutumiwa watendaji na nyaraka za Serikali kuwa amehujuma mradi wa ujenzi wa sekondari ya Sunya iliyopo wilayani hapo na kuongeza kuwa hakuhusika kufuja fedha hizo
“Kazi ya diwani ni kuhamasisha maendeleo ya kata yake ili yaweze kusonga mbele, mimi sio mhasibu wa kamati ya mradi wowote ndani ya kijiji au kata sasa inakuwaje nituhumiwe kuhujumu mradi tena kwa kuandikwa kwenye makabrasha ya vikao vya Halmashauri”?
“Kamati ya fedha na mipango imepitisha na kubariki kuletwa taarifa hii kwenye kikao cha madiwani, naamini walioyaleta hapa wana uhakika ya walichokiandika na kwa bahati nzuri taarifa hii ni ya mkaguzi wa ndani wa Halmashauri aliyotumwa na mkurugenzi ningependa sheria ifuate mkondo wake”Alisema Bw. Briton
Hata hivyo Diwani Braitoni aliliambia gaeti hili kuwa tayari amekwisha kuwasiliana na wakili wake ambaye kwa sasa wamepanga kuandika barua maalumu (notes) ya siku ishirini na moja kwa mkurugenzi ya kuonyesha nia hiyo ya kumshitaki kwa kushindwa kutimiza matakwa ya diwani huyo kusafishwa ndani ya kata yake
Aidha hoja hiyo ilivuta hisia kwa wawakilishi hao wa wananchi kwa kumtaka diwani huyo awe na subira na kuacha uamuzi wake huo wakisema kuwa uchunguzi wa kina ufanyike zaidi kubaini ukweli ya suala hilo ambalo lina taswira ya kuchafuliwa kisiasa
Akizungumza hayo Diwani Kone Lembile wa kata ya Kijungu alisema hakuna haja ya Diwani huyo kuhamaki kwani kama jambo hilo sio kweli haliwezi kuleta madhara kwake, lakini kama atakuwa amehusika hapo ndipo shida inaweza kutokea
Akiendelea na hoja hiyo huku akikatishwa na diwani huyo Lembile alisema, wananchi kwa nafasi zao nao hupima kinachozungumzwa na kumtaka diwani huyo kupuuza kauli hiyo ambayo inaonekana kuwa huenda kweli imemchafua kiasiasa
Hata hivyo hoja hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa Halmashaur i ya wilaya Mainge Lemalali kwa kumwomba Diwani huyo kuacha uamuzi huo akisema kuwa atahakikisha jengo hilo linakamilishwa na kuachana na mvutano huo wa kisiasa
“Mhe. Briton tukiachana na suala la umri nakusihi achana na uamuzi wako huo, kwani haya yataweza kuchelewesha maendeleo ya wananchi wakati tunaweza kukaa chini sisi na kutafuta ufumbuzi, ili mwisho wa siku tuone maendeleo ya wananchi yanasonga mbele”alisema Lemalali
Kauli hiyo ilizidi kuchochea hasira kwa diwani huyo na kutoa uamuzi wa mwisho kuwa mkurugenzi huyo apite katika vitongoji na vijiji katika kata yake hiyo ya Sunya kuelezea kuwa diwani huyo hakufuja fedha jambo ambalo mkurugenzi huyo hakulifanya
Hata hivyo gazeti hili lililazimika kuongea na mkurugenzi kuhusiana na tuhuma hizo na kusema kuwa ameshangazwa na uamuzi wa Diwani huyo wa kutaka kumfikisha mahakamani na kuongeza kuwa akiwa kama katibu wa madiwani hao atahakikisha kuwa wanayamaliza
Kuhusu kupita kwenye kata yake kutangaza kuwa diwani huyo hakuhusika na ufisadi mkurugenzi huyo alisema kuwa ni mapema na wala jambo hilo sio kubwa kama linavyo tafsiriwa na baadhi ya watu hasa wakidhani kuwa suala la kumfikisha mkurugenzi mahakamani ni rahisi
No comments:
Post a Comment